Vifaa zaidi vya uchunguzi vyahitajika kuongezeka katika bandari ya Malindi kukabiliana na Corona

0

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema vifaa zaidi vya uchunguzi wa maradhi ya Korona vinahitajika kwa wananchi wanaoingia na kutoka katika bandari ya Malindi Zanzibar ili kukabiliana na wingi watu wanaingia katika bandari hiyo.Naibu waziri ujenzi, mawasiliano na usafirishaji, Mhe. Mohammed Ahmada Salum amesema serikali ina wajibu wa kuhakikisha wakati wowote wananchi wake wanakuwa salama hivyo ni vyema kuona huduma zote zinahitajika katika kuimarisha usalama huo.

Amesema eneo hilo linatumiwa na watu wengi hivyo ni muhimu kuimarisha mazingira ya maeneo hayo kwa kuongeza vifaa na maeneo ya kuhifdhia watu watakaobainika kuwa na dalili za maradhi hayo.

Amevitaja baadhi ya vifaa na miundombinu inayohitajika katika maeneo hayo amesema ni pamoja na mahema, vyoo, mashine za kufanyia uchunguzi na vitu vingine vinavyohitajika katika eneo hilo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Kapten Abdallah Juma Abdallah amesema shirika hilo litasaidia ununuzi wa baadhi ya vifaa vya kuchunguzia maradhi hayo ikiwemo mashine za kupimia joto.