Ubalozi wa Uswiss watoa mchango wa Mil. 260 kwa tamasha la Sauti za Busara

0

Ubalozi wa Uswiss nchini umechangia zaidi ya shilingi milioni 260 ili kuwezesha Tamasha la Muziki la Sauti za Busara Zanzibar kwa miaka mitatu ijayo. Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Florence Tinguely Mattli, akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Busara Promotions Mhe. Simai Mohammed Said kwa ajili ya makabidhiano katika ofisi za Ubalozi jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Uswiss Nchini Tanzania Balozi Tinguly Mattli akimkabidhi mfano wa cheki ya shilingi milioni 260 Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Sauti za Busara Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said, hafla hiyoo ya makabidhiano imefanyika katika ukumbi wa Ofisi za Ubalozi wa Uswiss Jijini Dar es Salaam.

“Uswisi imekuwa ikisaidia matukio na juhudi mbalimbali katika sekta ya sanaa na utamaduni nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka kumi sasa,” alisema Balozi Tinguely Mattli. “Tamasha la Sauti za Busara ni mfano mzuri wa tukio kitamaduni ambalo huleta watu pamoja ili kufurahia kazi za sanaa na wakati huo huo kuchangia maendeleo ya kiuchumi.”

Mheshimiwa Simai alitoa shukrani kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya Busara Promotions kwa msaada huo. “Mashirika ya sanaa na utamaduni yanategemea sana ufadhili wa wadau wa maendeleo. Tunashukuru Ubalozi wa Uswisi kwa mchango wao katika kuwezeshaea kufanikisha tamasha hili,” alisema.

Tamasha la Sauti za Busara litaanza tarehe 9 na kufikia tamati tarehe 12 Februari 2017 katika ukumbi wa kihistoria wa ‘Old Fort’ mjini Stone Town, Zanzibar.