Maoni yetu: Sauti za Busara, tamasha la kimataifa ambalo wasanii wa nyumbani hawalio

0

Leo nimejisikia kuronga jambo kwa nia njema na kwa kushangazwa kwangu. Sauti za Busara ni  tamasha la kimataifa linalofanyika hapa nyumbani zanzibar kila mwaka hakuna asiyelijua, mataifa kwa mataifa hufunga safari kuja kushuhudia tamasha hili na wasanii kila kona ya dunia wanalililia kushiriki katika tamasha hili.

Lakini wako wapi wenyeji wa tamasha hili mbona siwaoni kwa wingi, wenyeji hawa ninaowazungumzia mimi si tu watanzania bali zaidi ni wasanii wa zanzibar. Tena wale tunaoitwa kizazi kipya tumekutwa na nini? Sitaki kuamini kwamba hatujui ukubwa wa hili tamasha au umuhimu wake sio kweli, tunajua. Huenda ukawa unajiuliza vipi na huku wanabaniwa? nikupe jibu kwa ufupi hapana hawabaniwi utanielewa muda sio mrefu.

Niseme ukweli tumezidi kuwa nyuma katika mambo ya msingi mambo ya kukuza biashara yetu na tumekuwa mbele kwenye mambo ya kuangusha muziki. Mimi kumbukumbu zangu nawakumbuka wasanii wachahe sana kushiriki kwenye hili tamasha kama Zeetown Sojaz Snipers (2015), Rico Single (2015,2017) na  Zenji Boy ambaye mpaka sasa ufuatiliaji wangu unaniambia ndio msanii pekee atakaye panda jukwaa la busara linalotarajiwa kuanza 16/2/2020 panapo uzima, Na wapo wengine wasanii wa miaka ya nyuma walishiriki katika tamasha hilo lakini kwa sasa muamko umekuwa mdogo.

Kikwazo ni nini? Narejea tena ni kizazi kipya tu. Najua Siti and the band wapo, bendi bora kwangu niipendayo Mapanya band, sisi wengine tatizo ni nini?

Utaratibu wa Sauti za Busara upo wazi kama matamasha mengine ya kimataifa unaomba kushiriki mtandaoni (online), na msanii pekee ambaye alikuwa amepewa nafasi ya upendeleo kila mwaka hushiriki bila ya maombi katika tamasha hilo ni marehemu bi kidude kutokana na heshima kuu aliyoiweka.

Mwaka 2017 na 2019 tulimuona Fid Q hakuna ubishi huyu ni msanii mkubwa Afrika Mashariki, na sisi pia ni wasanii wakubwa ndani ya zanzibar na tunaheshimiwa nini shida katika kuomba?

  1. Hatujui utumiaji wa mtandao kuomba?
  2. Sisi ni wakubwa sana kiasi cha kuona kuomba ni kujishusha?
  3. Au kushiriki kwa kutumia live band ndio shida?

Ni maswali ambayo nimebaki nikijiuliza na nakosa majibu sababu kama uwezo wetu wa mitandao kama ni ku-post, likes na comments tunaweza. Kwanini tusitafute watu wakutusaidia na kama tunakimbia live band tusahau kuwa wasanii wakubwa kimataifa.

Ndugu zangu mcheza kwao hutunzwa, wenzetu wa filamu kila siku wanatukimbia katika kushiriki katika matamasha makubwa. Leo nikiwa nayaandika haya, kuna vijana kutoka hapa hapa visiwani  ndugu Muddy Sule Mwanahisabati na Eddie Salum TZ, wanaelekea Kenya kwasababu ya kutumia mtandao na wanawania tuzo ya filamu huko.

Hebu tuamkeni na tuelewe ya kuwa hili tamasha ni zaidi ya Fiesta au Wasafi kutokana na ukubwa wake duniani. Na tusipoamka huenda ikakutokea wewe msanii wa heshima katika tamasha hili kama ilivyokuwa kwa Bi Kidude

Zenji255 inapenda kumpongeza Ison na uongozi mzima wa Stone Town Records.