Categories
Z! Extra

“Serikali ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Serikali ya Ras Al Khaimah” – Rais Dk. Shein

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Serikali ya Ras Al Khaimah katika kuanzisha programu ya mafunzo kwa walimu wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein ameyasema hayo leo wakati alipokutana na ujumbe wa Taasisi ya Sera na Utafiti ya Sheikh Saud Bin Saqri Al Qasimi huko katika ukumbi wa Hoteli ya Waldorf Astoria iliyopo mjini Ras Al Khaimah.

Ujumbe huo umekuja kufuatia agizo la Mtawala wa nchi hiyo alilolitoa kwa Msaidizi wake wa masuala ya elimu siku ambayo Mtawala huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. Shein katika ukumbi wa Kasri yake iliyopo Aldhait mjini Ras Al Khaimah.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein ameualika uongozi wa Taasisi hiyo kuja Zanzibar kwa lengo la kukutana na uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili kuona jinsi gani wanaweza kushirikiana katika kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu wa Zanzibar.

Rais Dk. Shein ameeleza kuwa hatua hiyo itaiwezesha Wizara ya Elimu kutoa vipaumbele vya mahitaji waliyonayo ili iwe rahisi kutekeleza programu hiyo jambo ambalo litaisaidi Taasisi hiyo kutambua vipaumbe vya Zanzibar na hatimae kurahisisha utekelezaji wa programu hiyo.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Sera na Utafiti ya Sheikh Saud Bin Saqr Al Qasimi Natasha Ridge, ameeleza kuwa Taasisi hiyo pia, inajishughulisha na utoaji wa mafunzo ya kitaalamu ya kuwajengea uwezo walimu kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari.

Hata hivyo uongozi wa Taasisi hiyo uko tayari kuja Zanzibar mnamo mwezi wa Novemba mwaka huu kwa ajili ya kukutana na uongozi wa Wizara ya Elimu pamoja na uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili kuangalia vipaumbelea ambavyo wao wataweza kuvifanyia kazi katika kutoa mafunzo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.