Mwandishi habari Tanzania Erick Kabendera amepandishwa kizimbani

0


Mwandishi habari Tanzania Erick Kabendera amepandishwa kizimbani kusomewa mashtaka mapya matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi .

Katika mashtaka hayo Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja za kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.
Kwa mujibu wa mashtaka yaliowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyatekeleza hayo baina ya Januari 2015 na Julai mwaka huu mjini Dar Es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani leo.

Makosa yote hayana dhamana.


Mawakili wake wameondoa ombi la dhamana kutokana na mashtaka hayo mapya.

Akizungumza na waandishi habari punde baada ya Kabendera kusomewa mashtaka, wakili wake Jebra Kambole amesema

‘Wakati Erick anakamatwa siku ya kwanza aliambiwa kosa lake ni la uhamiaji, akapelekwa kwenye mamlaka za uhamiaji, akahojiwa, pasipoti yake ikachukuliwa. Uhamiaji wakamkabidhi kwa jeshi la polisi makao makuu Central Jeshi la Polisi wakamhoji kwa makosa ya uchochezi.

‘Kuanzia hapo hajawahi kuhojiwa kwa makosa mengine zaidi ya hayo’ amesema Jebra Kambole.

Amefafanuwa kwamba kutokana na kwamba mashtaka aliyosomewa Kabendera hayana, dhamana ameshindwa kutoka leo.
‘Tunachofanya sasa, ni kuangalia upelelezi unafanyika kwa wakati’ ameeleza Wakili huyo.

Kesi dhidi ya Erick Kabendera inatarajiwa kusikilizwa Agosti 19.
Erick Kabendera mwandishi habari anayeandika magazeti ya ndani na nje ya Tanzania alikamatwa Jumtatu 29 Julai wiki iliopita na watu waliojitambulisha kuwa ni maafisa wa polisi.

Katika mkutano na vyombo vya habari, kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar Lazaro Mambossasa amesema kuwa mshukiwa huyo alikaidi agizo la polisi la kufika mbele yao kwa ajili ya mahojiano.

”Mwandishi huyu aliitwa hakutekwa lakini kwa ujeuri alikaidi wito huo…. kimsingi pengine iwapo angewasili angehojiwa na kuachiliwa”, alisema Mambossasa