Mwanafunzi Askari Chuo cha Anga cha (JWTZ) Ajiua Kwa Kujipiga Risasi

0
Mwanafunzi wa Chuo cha Anga (SKUA) cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichopo Kange jijini Tanga, Philip Fred (28) amejiua kwa kujipiga risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Leonard Paul aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kwamba tukio hilo ni la jana May 10, saa 1.15 usiku katika chuo hicho kilichopo kata ya Maweni nje kidogo ya jiji.
Alisema askari mwenye cheo cha Koplo mwenye namba MT 81627 alijiua wakati akiwa katika eneo la lindo chuoni hapo.
“Kimsingi chanzo cha kifo cha askari jeshi huyo bado hakijajulikana na imefahamika kwamba alikuwa ni mwanafunzi wa ‘Level one’ chuoni hapo na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Bombo”, alisema Kamanda.
Katika tukio jingine Kamanda alisema askari wanamshikilia mkazi wa mtaa wa Mgwisha, kata ya Pongwe jijini Tanga, Masudi Hamis (22) kwa tuhuma za kukutwa na sare moja ya askari wa JWTZ.
Source: Mpekuzi Huru