Kimbunga yapigwa faini na ZFA baada ya kupewa kadi za njano 5 mchezo mmoja

0

Timu ya Kimbunga kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja imekuwa ndio timu ya mwanzo msimu huu kupigwa faini kwa kosa la kuoneshwa kadi za njano wachezaji wao watano katika mchezo mmoja.

kimbunga

Faini hiyo ni Shilingi Elfu 50 kutokana na wachezaji wake kuonyeshwa idadi ya kadi nyingi za njano kwenye mchezo mmoja ambapo kwa mujibu wa Kanuni ya kuendeshea mashindano ya ligi kuu Visiwani Zanzibar, Kifungu cha 16 (d) kinatoa adhabu ya faini ya Shilingi Elfu hamsini za Kitanzania kwa timu itakayoonyeshwa kadi za njano wachezaji wake watano kwenye mchezo mmoja.

Wachezaji waliosababisha timu yao kupigwa faini ni Idrissa Simai Pandu, Juma Simai Shukuru, Nyange Khamis Mtumwa, Khamis Hamada Mwevura pamoja na Haji Nahoda Haji ambao wote wameoneshwa kadi hizo katika mchezo wao dhidi ya Kijichi uliochezwa siku ya Alhamis tarehe 13/10/2016 mchezo ambao Kijichi ilishinda 3-1 ndani ya dimba la Amaan.

Mbali na adhabu hiyo pia Kimbunga itapata wakati mgumu katika mchezo wao wa Jumatatu dhidi ya Miembeni kufuatia adhabu ya mchezaji wao Khamis Hamada Mwevura mwenye kadi tatu za njano mfululizo alioneshwa katika michezo yao.

Mwevura alianza kuonesha kadi ya njano katika mchezo wao wa awali timu yake ilipolala kwa mabao 2-1 dhidi ya Mundu mchezo uliochezwa tarehe 02/10/2016 katika dimba la Amaan.

Katika mchezo wao wa pili Mwevura pia alioneshwa kadi ya Njano walipofungwa na Zimamoto bao 1-0 mchezo uliosukumwa Fuoni siku ya Ijumaa tarehe 07/10/2016.

Na kadi ya njano ya tatu alioneshwa katika mchezo wa Kimbunga dhidi ya Kijichi uliochezwa siku ya Alhamis tarehe 13/10/2016 mchezo ambao Kijichi ilishinda 3-1 ndani ya dimba la Amaan.