Herrera ataka kusalia United, aitolea nje Barcelona

0

Kiungo wa Manchester United Ander Herrera ametoa ishara kuwa anataka kufanya mkataba mpya na Mashetani Wekundu wa Old Trafford.

Mapema mwezi huu, ilidaiwa kuwa Herrera ni miongoni mwa wachezaji walioko kwenye rada za Barcelona. Ernesto Valverde ambaye alifanya kazi na Herrera katika klabu ya Athletic Bilbao akitajwa kumtaka mchezaji huyo Camp Nou baada ya kurithi nafasi ya Luis Enrique.

Kwa mujibu wa The Telegraph, Herrera mwenye umri wa miaka 27, badala yake anataka kujitia kitanzi Manchester United baada ya kampeni nzuri katika Old Trafford msimu huu.

Tangu kutua kwa Jose Mourinho mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania amekuwa moja ya majina ya kikosi cha kwanza na amejizolea tuzo ya mchezaji wa mwaka katika klabu yake.

Herrera ameanza mechi 44 katika michuano yote kwenye kampeni za mwaka 2016-17 ambapo sasa amebakiwa na miezi 12 tu katika mkataba wake na hivyo kuifanya Barcelona kutumia wakati huu kumshawishi kutua Camp Nou, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kujaza mkataba mpya United.