Fahamu: Mohammed Issa Haji ‘Matona’

0
matona
Mohammed Issa Haji Matona amezaliwa mnamo mwaka 1969 katika kijiji cha Paje, Zanzibar, ambacho kipo maili 45 kutoka Stone Town.

Alianza elimu yake ya msingi katika miji ya Zanzibar na Morogoro lakini alikuwa akipoteza muda wake mara nyingi katika kutengeneza muziki akiwa na umri mdogo. alishiriki katika mashindano mbali mbali ya mpira wa miguu na ya kukimbia, lakini alikuwa akipenda sana kupiga ngoma za asili na rafiki zake baada ya kutoka shule.

Baba yake, Issa Matona, ni mwanamuziki maarufu sana, katika uimbaji na upigaji wa ngoma za Kidumbaki na Taarab. Kazi ya muziki ya Matona ilianza kuonekana alipokuwa akiimba nyimbo zilizotungwa na baba yake. Alivutiwa kufanya kazi ya muziki kutoka kwa baba yake ambaye ndie aliyemfundisha. Majirani na marafiki waligundua kipaji chake na kumuongelea kuwa atakuwa mrithi wa baba yake baada ya kumsikia akipiga ngoma ambayo aliyoitengeneza yeye mwenyewe.

Mnamo mwaka 1986 aliondoka shule na kujiunga katika kundi la baba yake kama mpiga ngoma wake huko Dar es Salaam. Matona alirudi Zanzibar mwaka 1987 na kujiunga na kikundi cha Khasi Musical Club. Mwaka 1989 alianza shughuli za muziki na kujiunga na kikundi maarufu kijulikanacho kama Mohammed Ilyas and Twinkling Stars, akiwa kama mpiga ngoma, violin na qanun. Aliondoka katika kikundi hicho mwaka 1993 na kuamua kujiunga na Bwawani Taarab Orchestra akiwa kama kiongozi wa muziki wa kundi hilo. Hapo alikuwa mtunzi wa muziki, mwandishi vile vile mpiga qanun na mpiga kinanda.

Safari yake ya muziki haikuishia hapo bali iliendelea, mwaka 1995 aliondoka katika kundi hilo na kujiunga katika kundi kongwe hapa Zanzibar, Nadi Ikhwan Safaa (Malindi Taarab). Kwa upande mwingine wakati akiwa anaendelea katika kundi hilo aliweza kuanzisha kundi lake mwenyewe aliloliita kwa jina la G-Clef Taarab Orchestra, ambapo liliweza kupata umaarufu mkubwa na kujulikana kila sehemu na kuwavutia na kuwafundisha wanamuziki wadogo ambao waliokuwa wakipiga muziki aina ya ‘Modern Taarab’. Mwaka 2002, Chuo cha Muziki wa nchi wa Majahazi (DCMA) kilifungua milango yake na Matona mwenywe binafsi alijitolea kuwa mwalimu katika chuo hicho. Ili kujiongezea akili na kuutanua wigo wa elimu yake, Matona alienda kusoma mara mbili nchini Misri (Egypt) kwa masomo ya elimu ya juu ya muziki. Mwanamuziki huyo ambae mwenye uwezo wa kupiga vyombo vya muziki zaidi ya viwili, mwenye uwezo wa kutunga na kuandika nyimbo amesafiri mara kwa mara katika nchi mbalimbali duniani akifanya maonyesho yake. Matona alifaulu mtihani wake katika chuo cha Agder Music Academy kilichopo Norway.

Msikilize Matona akiwa ameimba moja ya tungo za baba yake mzee Issa Matona.

 Muangalie Matona akiwa na Kikundi kutoka chuo cha muziki cha DCMA, Zanzibar