Fahamu: Maisha na Muziki wa Haji Mohammed wa East African Melody

0

Haji Mohammed Omar alizaliwa Septemba 9, 1962 katika hospitali ya Mnazi Mmoja Unguja akiwa mtoto wa pili katika watoto tisa waliozaliwa na mzee Mohammed Omary.

Alianza darasa la kwanza katika shule ya msingi Darajani na Sekondari katika shule hiyohiyo ya Darajani mpaka kidato cha tatu mjini Unguja. Baadaye akamalizia elimu yake ya sekondari katika shule ya Shangani hapohapo Unguja mnamo mwaka 1979.

hj

Safari yake ya uanamuziki ilianza mwaka 1978 Zanzibar katika kikundi cha Taarab cha Razi ambacho kilikuwa mtaani kwao Vikokotoni mjini Unguja, baadaye akahamia bendi kongwe ya Nadi Ikhwan Safaa- Malindi. Wakati huo akiwa kijana mdogo akapikwa na kupikika kwenye muziki huo hasa upande wa kupiga vyombo na utunzi wa mashairi.

Baada ya kuiva katika kikundi cha Nadi Ikhwan Safaa akahamia kikundi kingine kikongwe cha muziki huo cha Culture ambacho kwa sasa ni chuo cha Taarab mjini Zanzibar ambapo yeye anatajwa kuwa miongoni mwa walimu waliofunda baadhi ya wanamuziki wanaotamba kwa sasa.

Haji anatajwa kuwa miongoni mwa watu walioanzisha Taarab ya kizazi kipya yaani Modern Taarab. Ambapo mwaka 1994 wakiwa falme za kiarabu Dubai, Haji akiwa na Mahmoud Alawi, Lamania Shaaban na Omary Mlamali, walianzisha kikundi cha East African Melody.

modern

Mvumo wa kikundi hicho kilifika mpaka pwani ya Afrika Mashariki ambapo kwa ajabu kubwa Melody ikawa na wapenzi wengi Afrika Mashariki kuliko huko kilipoanzishwa. Ndipo wakaamua kurudi nyumbani Zanzibar na baadaye wakahamia Dar es Salaam miaka 13 iliyopita.

Kwa mujibu wa katibu wa East African Melody, Abuu Ruwa ambapo Haji alikuwa mkurugenzi, Haji aliimba na kutunga nyimbo nyingi tangu alipoanza muziki na baadhi ni Karibu Habibi, Best Maridadi, Mambo yetu Bambam, Mavituz na Majamboz, Sitaki Nataka, Nitakufa kwa ahadi, Zilipendwa na nyingine nyingi ambazo zilifikia takriban nyimbo 50.

Kwa maneno yake Haji enzi za uhai wake alisema hajawahi kuona kiumbe anaeimba Taarab kwa ustadi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki kama Rukia Ramadhani.

Haji MohamedHaji alisema, aliwahi kutunga na kuuimba wimbo wa ‘Karibu Habibi’ lakini kwa kupenda kushirikisha watu katika sanaa akaamua kumjaribu Rukia Ramadhani auimbe wimbo huo. Basi kwa mara ya kwanza kuuimba aliuimba kwa ustadi kiasi akaona hata yeye hakuweza kuuimba kama alivyouimba Rukia, na akaamua urikodiwe upya na Rukia, hivyo ‘Karibu Habibi’ umerekodiwa mara mbili kwa heshima ya bi Rukia Ramadhani ambaye mpaka sasa anatamba katika tasnia hiyo.

Mpaka anaaga dunia April 16, 2013 katika hospitali ya Muhimbili kutokana na shinikizo la damu, Haji mohammed alifanikiwa kupata watoto watatu Mohammed, Ummy na Salama.

Aidha alifanikiwa kuoa wake wawili ambao wametajwa kwa jina moja moja la Fetty na Rahma ambao alitengana nao, inatajwa na ndugu zake wa karibu kuwa mpaka anafariki hakuwa na mke.

Sikiliza Baadhi ya nyimbo Marehemu Haji Mohammed alizowahi kuimba akiwa na East African Melody enzi za uhai wake

Chanzo: Kido Jembe Blog