David Burhan kuzikwa leo Iringa Mjini

0

ALIYEKUWA kipa wa Kagera Sugar, Marehemu David Burhan anatarajiwa kuzikwa leo Jumatano (Feb. 1) nyumbani kwao Iringa Mjini ambapo leo mwili wake tayari umeshasafirishwa kutoka Hospitali ya Bungano jijini Mwanza kwenda kwao.

burhan

Burhan alipatwa na umauti usiku wa kuamkia juzi Jumatatu akiwa anapatiwa matibabu kwenye hospitali hiyo ambapo ndugu wa marehemu walidai kuwa ndugu yao aliwataarifu kuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa manjano kabla ya kupatwa na kifo hicho.

Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein amesema Burhan atakumbukwa kwa mambo mengi aliyoyafanya katika klabu yao pamoja na soka kwa ujumla ingawa kikosi chao kimeshindwa kusafiri kwenda kumsindikiza mwenzao maana hawakujua ratiba sahihi ya mazishi.

Mohammedi alisema walipenda timu nzima ikamzike Burhan ila walikuwa hawajaambiwa ni lini familia imeamua kumzika Burhan hivyo wachezaji wawili wameiwakilisha timu ambao ni Babu Ally na Juma Mpola ambao walikuwa rafiki wakubwa wa marehemu na waliishi chumba kimoja.

Imetayarishwa na: Ali Khamis