Chidy Grenade, Baba Rhino: Chipukizi wa kuwaangalia kwa mwaka 2017

0

Katika muendelezo wa kuangaza vipaji vipya vya muziki muhimu kuviangalia kwa mwaka huu 2017, tunakuletea vijana wawili ambao wamefungua mwaka kwa mafanikio makubwa, na wameonesha uwezo wake mkubwa juu ya sanaa yao ya muziki.

Chidy Grenade

kwa kipindi kirefu alikuwa akifanya muziki wake visiwani Zanzibar ila muda wa muziki wake kuonekana visiwani hapa ulikuwa bado. Katika moja ya jitihada ya Chidy alifanikiwa na itakayomfanya aendelee kujikaza zaidi ni baada ya kuachia wimbo wake mpya ‘Nalia na Nani’ akiwa chini ya usimamizi wa uongozi wa Tausi Talent. Wimbo huo ulipata nafasi ya kutambulishwa video yake katika kituo cha MTV BASE East.

“Kwanza sio mimi tu, hata watu wangu wa Zanzibar walifurahi. Na kiupande wangu nilifurahi zaidi kuona MTV Base East wamenipa shavu la kuitambulisha video yangu kwenye kituo chao na ninawaahidi mashabiki wangu nitakaza zaidi na kufanya muziki mzuri upite kila pande ya dunia tuzidi kuutangaza muziki wetu wa Zanzibar” Amesema Chidy Grenade.

Baba Rhino

Kwa mara ya kwanza nilikutana na Baba Rhino akiwa studio mwishoni mwa mwaka 2016 anatengeneza wimbo wake aliouachia hivi karibuni na alionekana akiwa na matumaini mengi juu ya wimbo wake kufanya vizuri endapo atautambulisha kwa mashabiki.

Waswahili wanasema “Asiyejituma na asile”, jitihada za msanii huyu zilionekana kila sehemu sio Zanzibar tu, kwani alihakikisha anasambaza wimbo na video yake katika vituo vyote vya redio na TV za Tanzania ili mashabiki wamtambue ujio wake mpya.

“Jitihada Wajada, Siwezi sema kwamba ni jitihada zangu peke yangu ila mungu ndie muweza wa kila kitu. Nashukuru wimbowa ‘Muda’ umepokelewa vizuri sana, Sasa hivi nipo katika matayarisho ya kutoa wimbo mwingine na siwezi sema lini nitaachia kwani ‘Muda’ bado inafanya vizuri, kikubwa ni mashabiki wasubiri ujio mwingine mpya” Amesema Baba Rhino.

Angalia video za wasanii hao:

Chidy Grenade

Baba Rhino