Baby J azungumzia kuhusu ukimya wake na mipango mipya ya kuwasaidia wasanii wa kike Zanzibar

0

Ikiwa mwaka 2016 unaendea mwishoni kuna wasanii hupenda kuachia nyimbo za kufungia na kufungulia mwaka lakini kwa msanii wa kike Baby J imeonekana ni tofauti kwake baada ya kuonekana kuwa kimya muda mrefu toka aachie kazi yake ya mwisho ‘Nimempenda mwenyewe’.

baby jAkiongea na Zenji255 Baby J amesema kuwa ameamua kukaa kimya kwa muda mrefu ili kujiandaa upya kwa ajili ya kuufunga na kuufungua mwaka 2017.

“Naweza kusema ukimya wangu una sababu, unajua kila mtu ana mipango yake katika maisha na ukiachilia sanaa ninayoifanya ila nina mambo yangu binafsi vile vile nayafanya na ndio yaliyonifanya nikae kimya kwa muda. Nimeamua kufanya hivyo kwanza, ni kupumzika. Pili, kuuangalia muziki wetu wa Zanzibar unapoelekea kwa sasa na nini natakiwa nifanye nikirudi kwenye kazi yangu.” Amesema Baby J.

Kwa upande mwingine Baby J alizungumzia kuhusiana na mipango ya kuwasaidia wasanii wa kike Zanzibar ambao wapo katika sanaa ya muziki lakini hawajui wapi kuanzia.

“Nia ya kufanya jambo hilo ninayo na kwa sasa najaribu kutafuta msaada na kama nitafanikiwa kuupata nitafungua kama kituo cha kuwasaidia wasanii wa kike Zanzibar. kwani wasanii wengi wao wa kika hapa Zanzibar wamepita kwenye mikono yangu lakini lengo la kuwasaidida ninalo kikubwa ninachowataka wasikate tamaa na kama wanahitaji msaada wowote kutoka nitakuwa nao pamoja.”